Home » Articles » EDUCATION

MAKALA MUHIMU KWA ALIYEFELI MTIHANI

MAKALA MUHIMU KWA ALIYEFELI MTIHANI

Kila mwanzo wa kufeli ndio hatua ya kujipanga vema

 

Ni masikitiko makubwa ambayo umeyapata kwa kuanguka kimasomo. Wengi wamelia sana, wengi wamepata mshtuko na wengine kudiriki hata kujiua. Kumbuka kuwa kila linalotokea limeshaandikwa kuwa litatokea na hivyo hakuna awezaye kubadilisha majaliwa ya mungu.

 

Sasa hebu angalia ni hali gani unayosikia ndani ya moyo wako kwa kuanguka katika mitihani yako, je unapaswa kulaumiwa? Kwa upande huu haipaswi kulaumiwa kwani ndiyo unazidi kupandikiza ugonjwa juu ya ugonjwa na anayekulaumu anaweza kukuletea athari za kisaikolojia.

 

Napenda kusema kuwa, hapa ndiyo unaanza safari yako katika maisha mapya kwani siku zote afanyaye kosa ndiye anayejifunza zaidi kuliko ambaye hujawahi kufanya kosa. Tena jambo la kushukuru ni kwamba umepata changamoto hii mapema kabla hujafika mbali hivyo itakusaidia sana kurekebisha lile tatizo la mwanzo na kuwa makini na masomo ya mbele.

 

Kufeli mtihani ni sawa na kukosolewa kwa kitu au kazi uliyoifanya. Wengi huchukia sana wanapokosolewa lakini ukifanya uchunguzi utaona kuwa aliyekosolewa hubadilisha njia ya kufanya ile kazi ili apate kufanikiwa na kile alichokosolewa nacho. Hivyo utaona kama mtu alifeli basi atajipanga upya kimasomo ili afanikiwe hapo baadaye.

 

Wengi hujiuliza, "mimi umri wangu mbona unaenda? Kweli nitamaliza kusoma na leo?”. Wengi sana hiyo ndio sababu ya kuumia kwao. Lakini umeshatembelea vituo vya elimu ya juu kama vile vyuo vikuu? Huko utaona watu wazima ambao una uwezo wa kuwaita baba na bado wako wanatafuta elimu.

 

Hutakiwi kulaumiwa kwa kufeli kwako, na ni kosa kubwa mtu akilifanya kwa kukulaumu kwani atakuwa hakujengi kimaisha na mawazo na hatimaye anakubomolea malengo yako.

 

Ni vema kutokata tamaa na malengo yako. Jitahidi sana kuyaweka akilini malengo yako hata kama ulitaka kuwa daktari au mwalimu au mhandisi basi endelea na lengo hilohilo kwani elimu haina mwenyewe bali ni juhudi za mtu yeyote.

 

Je umeshawahi kuwauliza madaktari wakubwa? Umeshawauliza walimu kuhusu historia zao za nyuma kimasomo? Umeshawauliza wahandisi, wahasibu na wataalamu wa mambo mbalimbali? Utaona baadhi yao walifeli mitihani yao huko nyuma lakini kwa kuwa hawakukata tamaa na kuendelea kuyaweka malengo yao akilini, leo hii wamefanikiwa na wako makazini wakisubiri mishahara yao mwisho wa mwezi.

 

Ukataji wa tamaa na kubabaisha malengo yako ndiyo kutakuumiza sana na ni jambo hatari ambalo unapaswa uepukane nalo. Wazazi wengi wanaofahamu hili hutaona hata siku moja wakiwakaripia watoto wao walioanguka katika mitihani yao. Na utawaona wakitumia njia mbadala ya kuwasaidia ili wasirudie makosa hayo.

Kwa hakika kabisa kuna wanafunzi waliofaulu kwa alama za juu sana kidato cha nne lakini kutokana na kubweteka huku wakajikuta wakianguka katika kidato cha sita. Na wewe uliyeanguka kidato cha nne, ukajitahidi kurekebisha ratiba zako ukarudia kufanya mtihani, leo hii umefaulu.

 

Ninachopenda kuwashauri ni kwamba, usisikitike kwa kuanguka huku, huu ni mwanzo. Rekebisha staili yako ya kwanza ya kimasomo na ratiba zako. Usirudie mtihani wako kwa kutumia mtindo uleule wa kujisomea kama mwanzo. Badili aina ya kujisomea na kama hujui ni aina gani ya kujisomea basi jaribu kutaka ushauri kwa wakubwa ujue ni njia gani sahihi za kutumia ili usirudishe majibu yako kama ya nyuma.

 

Ni vema ukatengeneza ratiba yako kulingana na mazingira unayoishi kwa maana mazingira yanachangia sana kwa mwanafunzi aidha kufaulu au kufeli. Na ukarudia mtihani wako kwa staili ileile ya mwanzo basi una hatari ya kufeli kila mwaka kwani hakutakuwa na mabadiliko yoyote.

 

Pia kikubwa napenda kukukumbusha kuwa jitambue kuwa wewe ni nani na unahitaji nini na una malengo gani. Hilo ndio jambo zuri sana kwani wanafunzi wengi leo hii hawajui wajibu wao na hawana malengo yoyote yale. Wao wanasoma tu kukamilisha ratiba basi!

 

Jambo zuri napenda kuwashauri pia wazazi kutowakatisha tamaa watoto wao walioanguka, wasiwakaripie bali waongee nao kwa utaratibu kuwafahamisha matatizo yao waliyoyafanya kama vile kutojisomea, kuzidisha michezo na mambo mengine. Na wakae chini kujadili ni jinsi gani wafanye ili kurekebisha tatizo hili kwa kubadilisha mwendo mzima wa kujisomea.

 

Huenda wale wanaojiua hufanya hivyo kwa kukosa raha ya kukaripiwa na kutupiwa maneno machafu haya na yale na kujiona hawana thamani tena duniani. Hivyo tujiepushe kwani hii ni dhima kubwa sana.

 

Kama unalolote la kuongeza hapa au kama una ushauri na maswali yoyote basi jisikie huru kutuandikia katika kisanduku hapo chini au katika ukurasa wetu wa maswali na majibu kwani huu ni mtandao wako na ni haki ya kila mtu anayetaka kujua jambo linalomsumbua na kulipatia ufumbuzi wake. tuko kwaajili yenu katika kuwasaidia na kuendeleza jamii yetu. Ahsante.


Category: EDUCATION | Added by: Admin (01/Jun/2013)
Views: 647 | Tags: jitihada, education, elimu, feli, makala, matokeo, mtihani, muhimu | Rating: 0.0/0
Total comments: 0
Name *:
Email *:
Code *: