Home » 2017 » December » 23 » Alibaba na wezi 40 Part 15
08:58
Alibaba na wezi 40 Part 15

SEHEMU YA KUMI NA TANO

ALIBABA NI TAJIRI

 

Kutoka sehemu ya kumi na nne:

Baada ya kiongozi wa wezi kujulikana na Marjane baada ya kuingia ndani ya nyumba, Marjane aamua kutumia njia za ujanja na kufanikiwa kumwua. Alibaba alifurahi sana na kuamua kumuomba mwanaye Khalid amuoe Marjane iwe ni kama zawadi kwake, naye Marjane kwa upole akakubali........

Endelea sehemu ya Kumi na tano.

Hivyo basi, Khalid na Marjane wakafunga ndoa. Watu wengi walikuja kwenye sherehe. Wengi wao walikuwa ni majirani na rafiki zake Alibaba.

Katika sherehe hiyo, mmoja wa wageni alimwambia Alibaba, “Marjane ni masichana mzuri sana. lakini sio jambo la ajabu kweli kwa tajiri kama wewe kuamua mwanao amuoe mfanyakazi wa ndani?”

Kabla Alibaba hajajibu, mgeni mwengine akaingilia mazungumzo na kusema, “Marjane ni msichana mwerevu, mjanja, mpole na muaminifu. Hivyo Khalid hakuwa na haja ya kutafuta tajiri mwenzake, bali ni mwanamke bora, hivyo Khalid ana bahati ya kumpata Marjane.”

Alibaba alitabasamu kusikia hivyo na akachukua sahani nyingine ya halua na kuendelea kuburudika pamoja na wageni wake, hatimaye Alibaba alikuwa ni mtu mwenye furaha na amani.

Familia iliishi kwa furaha kwa miezi mingi. Khalid aliendelea na kazi yake ya kuuza mazulia na wanawake watatu walibaki nyumbani kwa kazi za nyumbani. Alibaba hakuwa tena mkata kuni kwani bado kulikuwa na dhahabu zaidi nyumbani kwake zilizobaki. Lakini daima alikuwa akifikiria kuhusu wale wezi arobaini na hazina zilizopo mle pangoni. Hazina bado zipo?

Mwaka mmoja baada ya ndoa, Alibaba alikuwa amekaa kwenye kistuli nje ya nyumba yake, ilikuwa ni jioni iliyotulia na alikuwa akitazama watu wakitembea huku na huko.

“Angalia watu wote hawa wanaoishi mjini hapa,” alijisemea moyoni. “huenda kuna wezi wengine kati yao. Najua kwamba wale wezi arobaini walishakufa, lakini hakuna wengine zaidi ya wale kweli? Huenda wakawa bado wapo na wanaendelea na tabia ya kuiba mali na kuzificha katika lile pango. Dhahabu zangu humu ndani zimebaki chache, na nahitaji dhahabu nyingine zaidi.” Aliendelea kufikiria. “Nitakwenda pangoni kuangalia.”

Baadaye wakati wanapata chakula cha jioni, Alibaba akamwambia mkewe kuhusu mpango wake.

“Nitakwenda kesho asubuhi sana,” alisema. “Nitakwenda na punda wangu.”

 

“Lakini unaweza kuwa hatarini,” alijibu mkewe. “Huenda kuna wezi zaidi ya wale arobaini. Wakawa na mikuki na visu vikali. Watakuua wakikuona!”

“Nitakuwa salama, mpendwa,” alijibu alibaba. “Usihofu kuhusu mimi.”

“Basi nenda na mwanao Khalid,” Mkewe alimshauri.

“Khalid ana kazi nyingi sana za kuuza mazulia dukani kwake,” Alibaba alijibu. “Nitakwenda pangoni mwenyewe kama nilivyoenda mara ya kwanza.”

Asubuhi iliyofuata, Alibaba aliamka mapema sana, akachukua makapu sita na kuyafunga kwa wale punda wake watatu. Kisha akaiaga familia yake na kuelekea msituni.

Alipofika katika jiwe kubwa la lile pango, alisimama na kuangalia maeneo yaliyozungula pango lile. Aliuona mti mrefu ambao alijificha mara ya kwanza alipogundua pango lile. Alisikiliza kwa makini sana – hakukuwa na sauti za kwato za farasi, wala sauti za wanyama wa porini, hakusikia wala kuona chochote ambacho kingemtia hofu.

Akavuta pumzi nyingi ndani na kusogea karibu na jiwe kubwa la lile pango.

Kisha aksema lile neno la siri, “Fungukaaaa sesmiiiii!!!!

Taratibu kabisa, lango likafunguka na Alibaba akaingia ndani. Akaona sehemu ambayo aliuona mwili wa kaka yake. Alibaba aligeuka haraka sana ili asipatazame sana mahali pale kwani kungemtia huzuni zaidi. Akaendelea kwenda ndani zaidi.

Pango bado lilikuwa na hazina nyingi sana, dhahabu, fedha, sarafu, pete, bilauri za rangi ya fedha na hazina nyingi zaidi ya hizo – kitu ambacho hakukiona pale ni vitambaa vya hariri.

Alibaba akafikiri kidogo.

“Khoja Hussein!” alijisemea moyoni. “Kiongozi wa wezi alijifanya mfanya biashara mkubwa wa vitambaa vya hariri na kufanya urafiki na mwanangu! Alijaza duka vitambaa vya hariri – kumbe vilitoka humu pangoni.”

Alibaba akaendelea kuangalia hazina zote.

“Hakuna mtu aliyekuwepo humu kwa muda mrefu sana,” Alijisemea. “Nafikiri wezi wote wameshakufa. Hazina hii yote ni yangu!”

Hivyo basi, akachukua baadhi ya mifuko ya sarafu za dhahabu, na baadhi ya vito pamoja na bilauri nzuri zenye kung’aa.

“Hizi bilauri zitapendeza sana zikiwa mezani kwetu.” Alifikiri. “Mke wangu atazipenda sana.”

Alibaba akazibeba hazina hizo alizokusanya na kuzijaza katika makapu yake sita yaliyobebwa na punda wake.

“Hii inatosha kwa sasa,” alijisemea. “Sitaki kuwa mroho sana.”

Kisha katoka nje ya pango na kusema neno la siri, “Fungaaaaa sesmiii!!

Jiwe kubwa likajifunga na likaonekana kama mawe mengine tu ya pale msituni.

Wakati jua linakaribia kuzama, na mbingu inabadilika rangi na kuwa kama zambarau iliyokoza, Alibaba na punda wake wakaondoka kurudi nyumbani.

Hazina iliyochukuliwa na Alibaba ilidumu kwa mwaka mwingine zaidi. Wakati huu, Marjane na Khalid walipata mtoto wa kiume na Alibaba akaamua kumpa Khalid siri ya lile pango.

“Wewe ni baba sasa, Khalid,” Alibaba alimwambia mwanae. “Kuna kitu nataka kukuonesha – kitu muhimu sana. Unajua kwamba nina dhahabu, na unajua kwamba nilizipata kutoka kwa kundi lile la wezi. Wale waliokuwa wanataka kuniua.”

“Ndio baba,” Khalid alijibu. “Marjane wangu mwerevu aliwaua! Na ninajua kwamba dhahabu zile ndizo zilizokutajirisha.”

“Ndio, haswaa!!” Alibaba alisema. “Lakini sasa, nimezitumia nyingi sana, na sasa nahitaji nyingine zaidi. Nataka nikupeleke kwenye pango ambalo dhahabu hizo zinapatikana, Khalid. Siku moja wewe au mwanao mnaweza kuhitaji kujua mahala zilipo.”

“Ahsante sana, baba,” Khalid alijibu. “Nina furaha kwa kuniambia hivyo. Nilikuwa nashangaa hizi dhahabu mahali zinapotoka.”

Siku iliyofuata, Alibaba na mwanae wakafunga safari ya kuelekea msituni na walienda na punda wao watatu.

Kisha Alibaba akasema neno la siri, “Funguaaaa sesmiiii!!!”

Lango likafunguka, kisha Alibaba na mwanae wakaingia ndani.

Pango bado lilikuwa na hazina nyingi sana. Dhahabu zote pamoja na fedha na vito mbalimbali vilikuwa vinang’aa kutokana na mwanga unaoingia pangoni kupitia vitundu vya juu ya pango hilo. Khalid aliduwaa sana kuona hivyo.

“Siamini macho yangu!” alisema. “Kuna hazina nyingi sana!”

“Hakuna mtu aliyeingia humu kwa mwaka mzima sasa,” alisema Alibaba huku akiangalia maeneo yote ya pangoni mle. “Tutakuwa salama kabisa.”

Wakachukua baadhi ya hazina na kujaza kapu zao na kurudi nyumbani.

“Ahsante kwa kuniambia siri yako, baba,” Alisema Khalid wakati wanarudi nyumbani. “Mwanangu akiwa mkubwa, nitamwambia pia kuhusu hazina zile na nitampeleka huko pangoni.”

Alibaba alicheka kwa furaha. “Ndiyo,” alijibu. “Na yeye pia atamwambia mwanae.”

Familia ya Alibaba iliishi kwa amani na hawakuwa masikini tena.

****Mwisho wa Kisa hiki****

Kaa tayari kwa Kisa kijacho:

Sindubad katika safari zake saba(7)”

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 135 | Added by: badshah | Rating: 0.0/0
Total comments: 2
2  
The story was very very very interesting Mr Yahya you are the best smile

1  
MashaAllah....the story was very amazing, n interesting...i like marjane, she z very wise......

Name *:
Email *:
Code *: