Home » 2017 » December » 22 » Alibaba na wezi 40 Part 14
23:14
Alibaba na wezi 40 Part 14

SEHEMU YA KUMI NA NNE

UCHEZAJI WA MARJANE

 

Kutoka sehemu ya kumi na tatu:

Baada ya kiongozi wa wezi kujifanya mfanya biashara mkubwa pale mjini na kupata umaarufu. Sasa afanya urafiki na kijana wa Alibaba ambaye ni Khalid muuza mazulia. Kutokana na urafiki wao kuwa ni wa ukaribu sana na hatimaye kuaminiana sana. Sasa Khalid aamua kumkaribisha kiongozi wa wezi ndani kwao........

Endelea sehemu ya Kumi na nne.

Alibaba alipomuona mgeni yule, alitabasamu na kumpa mkono. “Karibu sana nyumbani kwangu,” alisema kwa ukarimu. “ Kijana wangu aliniambia mambo yote kuhusu wewe,” aliendelea kusema. “Najua wewe ni muuza vitambaa vya hariri muhimu sana hapa mjini na pia ni rafiki mkubwa kipenzi wa mwanangu. Yeye  ni kijana mdogo bado na anahitaji kujifunza mengi sana kuhusu mambo ya ulimwengu huu. Wazee kama sisi tunahitaji kuwaongoza vijana hawa katika njia nzuri.”

Khoja Hussein aliinamisha kichwa chake kisha akajibu.  “Kijana wako ni kijana mzuri sana, na ninafurahia sana mazungumzo yetu, matembezi yetu na pia tunapopata chakula pamoja. Lakini nina uhakika wewe ni mtu mwenye kazi nyingi sana, Alibaba. Ninaondoka sasa ili niwaache wewe na familia yako mkiwa wenye amani.”

Alibaba alimshika mkono. “Tafadhali bado usiondoke,” alisema. “Ningependa tukae hapa kwa muda huu ili tupate chakula cha jioni pamoja mimi, wewe, Khalid, mke wa Kassim na mke wangu. Marjane yuko jikoni anaandaa kuku mkubwa sana na ataweza kututosha sote.”

“Nashukuru sana kwa kunikaribisha,” alijibu Khoja Hussein. “Lakini nina tatizo kubwa sana. Siwezi kula chakula chochote chenye chumvi.”

Alibaba aliposikia hivyo, alishangaa sana. Ni ajabu sana kusema hivi!!

Alibaba akafikiria kwa muda mfupi, kisha akajibu. “Sawa, hilo halina tatizo. Nitamwambia mfanyakazi asiweke chumvi katika chakula chetu cha jioni leo.”

Kisha Alibaba alienda jikoni na kumkuta Marjane.

“Tuna mgeni kwaajili ya chakula cha jioni leo,” alimwambia. “Jina lake ni Khoja Hussein, ni mfanyabiashara mkubwa sana wa vitambaa vya hariri. Ni rafiki wa Khalid pia. Hawezi kula chumvi, hivyo usiweke chumvi katika chakula. Tafadhali pia pika mbogamboga – na kumbuka kutokuweka chumvi kwenye mbogamboga pia.”

“Sawa bosi,” alijibu Marjane. Kisha akanyamaza kidogo. “Huyu Khojha Hussein ni nani?” alijisemea moyoni. “Kwanini hali chumvi?” kisha Marjane akakumbuka usemi wa kizamani unaosema kwamba: ukitaka kumwua mtu, usile chumvi nyumbani kwake.  Ghafla Marjane akaingiwa na hofu. “Khoja Hussein amepanga kufanya nini?” alijiuliza. “Bosi wangu Alibaba yuko hatarini?”

Alipomaliza kuandaa chakula, alibeba sahani ya kuku mpaka mezani. Alipokuwa akiiweka mezani, Marjane alimuangalia Khoja Hussein kwa makini sana wakati akiwa anazungumza na Alibaba na mkewe.

“Huyu mtu mwenye ndevu ndefu nyeusi na upara,” Marjane alijisemea moyoni. “Lakini namtambua huyu mtu – ni kiongozi wa wezi – muuza mafuta – na sasa ni muuza vitambaa vya hariri!! Bosi wangu yuko hatarini tena – huyu mtu ana mpango wa kumuua bosi wangu usiku wa leo! Lazima nifikirie mpango madhubuti.”

Marjane akarudi jikoni na kuleta sahani ya mikate na bakuli kubwa la wali na mbogamboga. Alipokuwa akivitenga mezani, akamuangalia mgeni tena wakati akizungumza na Khalid na mke wa Kassim.

Ghafla Marjane akaona upanga. Ulikuwa umefichwa kwenye koti la mgeni! “amejaribu kuficha upanga,” Marjane alijisemea moyoni. “Lakini nimeweza kuuona.”

Alipokuwa anamalizia kutenga vyakula vilivyobaki, alizidi kufikiria zaidi kuhusu mpango wake.

Walipomaliza kula kuku, Alibaba akasema, “Kuleni matunda. Haya maembe ni mazuri sana.”

“Ahsante,” alijibu Khoja Hussein. Kisha akachukua embe moja kutoka kwenye bakuli na kuegemea kwenye kiti chake na kunyoosha miguu yake mbele na kutabasamu.

“Chakula cha leo ni kitamu sana,” alimwambia Marjane. “Wewe ni mpishi mzuri sana. Niambie, mbali na kupika nini kingine kizuri unaweza kufanya?”

Sasa Marjane akapata nafasi ya kutimiza mpango wake.

“Ninaweza kucheza,” Marjane alijibu. “Ungependa nicheze uone burudani wakati unakula matunda?”

“Unasema..??” alisema Khoja Hussein, akamgeukia Alibaba. “Je Marjane anaweza kucheza tumuone?”

Alibaba akatabasamu na kuitikia kwa ishara ya kichwa . Alikuwa na furaha kuona mgeni wake anaburudika jioni ile.

“Uhakika kabisa,” alisema Alibaba. “Na atatupigia dufu pia. Anajua sana kupiga dufu. Nenda kajiandae Marjane.”

“Sawa bosi,” Marjane alijibu.

Marjane akaenda chumbani kwake. Akavaa gauni refu la rangi ya fedha lenye kung’aa kwa juu. Akajifunga kitambaa mdomoni kuzunga kichwa chake. Akavaa mkanda mnene kiunoni. Kutoka kwenye mkanda ule akaweka ala ya kuwekea kisu, na katika ala ile akaweka kisu. Kisha akachukua dufu na kutoka chumbani kuelekea sebuleni kwaajili ya kucheza.

“Huyoooo amependeza!!” Alibaba alisema kwa furaha. “Sasa tutaburudika!”

Marjane akasimama katikati ya mlango na kuinama kidogo kama ishara ya kusalimia.

“Ingia! Cheza, Marjane!” Alibaba alisema kwa furaha. “ingia na ucheze! Mgeni wetu aone jinsi unavyojua kucheza!”

Marjane akaanza kupiga dufu taratibu na kuanza kucheza akizunguka chumba kile huku  akitabasamu.

Alibaba na mgeni wake wakaanza kupiga makofi na mke wa Alibaba na mke wa Kassim wakaanza kuimba. Khalid alisimama dirishani akitabasamu tu.

Kisha Marjane akaanza kucheza haraka haraka. Alionekana kama anataka kupaa. Gauni lake lilikuwa likizunguka kama mwamvuli. Alishikilia dufu juu kupita usawa wa kichwa chake na kulitikisa ili vikengele vidogo vya kwenye dufu lile vitoe sauti. Kisha, kwa mkono wa pili, akatoa kisu kilichopo kwenye ile ala aliyoifunga kiunoni kwenye mkanda. Akaonesha kama ishara ya kukatakata vitu hewani, zote hizo ni mbwembwe mbalimbali za uchezaji.

Akaendelea kucheza mpaka akaenda kwa Alibaba na kujinyooshea kile kisu kifuani kwake mwenyewe na kisha kumnyooshea bosi wake. Akaendelea hivyohivyo kucheza mpaka kwa mke wa Alibaba na kwa mke wa Kassim, na kisha kwa Khalid.

Akazunguka na kunyoosha kisu kile hewani juu na kuendelea kucheza.

Kisha akacheza mpaka kwa Khoja Hussein na kumyooshea kisu kama alivyofanya kwa wengine huku akishusha  dufu lile chini na kulishikilia kama sahani.

Alibaba alicheka na kutumbukiza baadhi ya sarafu za dhahabu kwenye lile dufu aliloshikilia Marjane.

“Unastahili kabisa kupata dhahabu hizi! Marjane” Alisema Alibaba. “Umetuburudisha vizuri sana jioni hii.”

Marjane huku ameshikilia dufu lile kama sahani ya chakula, akaendelea kucheza tena mpaka kwa wake wawili, nao wakatumbukiza sarafu za dhahabu katika dufu lile. Kisha ikawa ni zamu ya Khalid. Khalid alitabasamu wakati Marjane akimtazama na Khalid akatumbukiza sarafu za dhahabu kwenye dufu lile.

Mwishowe akafika kwa Khoja Hussein, Marjane akamuelekezea lile dufu.

Kiongozi wa wezi  alitabasamu na kuingiza mkono wake mfukoni ili naye atoa japo sarafu kidogo kama wenzake walivyofanya. Muda uleule, Marjane akanyanyua kisu chake juu hewani na, kwa nguvu zake zote alikisukuma kisu kile mpaka kifuani mwa Khoja Hussein.

Khoja Hussein akaanguka nyumba ya sofa. Alibaba na Khalid wakakimbia haraka kwenda kumsaidia.

Alibaba akaweka mkono wake mdomoni kwa Khoja Hussein kuona kama anapumua, na kisha akashika kiganja chake ili kuona kama mapigo ya moyo yanaendelea.

“Hapumui tena!” Alifoka Alibaba. “Na moyo wake umesimama! Amekufa!! Wewe muovu, msichana muovu kabisa!! Kwanini umemwua??”

Kisha Marjane akausogelea mwili wa Khoja Hussein na kuchomoa ule upanga uliokuwa umejificha kwenye koti. Akamuoneshea Alibaba.

“Hakuja kukutembelea.” Marjane alimwambia Alibaba. “Alikuja kukuua. Nimeokoa maisha yako tena bosi.”

“Alikuja kuniua?” Alibaba aliuliza kwa mshangao mkubwa sana. “Kwanini rafiki wa mwanangu Khoja Hussein aje kuniua?”

“Huyu sio Khoja Hussein.” Marjane alielezea. “Huyu ni yule kiongozi wa wale wezi thelathini na tisa. Ametaka kukuua muda mrefu sana. Huyu ni yule muuza mafuta ambaye alikuja hapa kabla – na ni muuaji huyu!”

“Kiongozi wa wezi? Wezi waliomuua kaka yangu? Lakini umejuaje Marjane?” Alibaba aliuliza. “umemtambuaje?”

“Uliponiambia kwamba hali chumvi, nikaanza kumtilia mashaka,” Marjane alieleza. “Nikakumbuka usemi wa zamani wa wazee wetu ukisema: ukitaka kumwua mtu, usile chumvi nyumbani kwake. Hivyo nilipoenda mezani kutenga chakula nikamuangalia usoni kwa umakini kabisa, nikamtambua kuwa ni yule yule muuza mafuta ila amebadilika kwasababu amenyoa upara na ameweka ndevu za bandia, pia nikaona upanga ameuficha katika koti lake. Unaona sasa! Nilikuwa na uhakika kabisa kuwa ndiye mwenyewe”

Alibaba alifurahi sana kusikia hivyo.

“Marjane, umeokoa maisha yangu tena,” alisema. “Wewe ni muaminifu sana, ni msichana mjanja, na kuanzia sasa nakupa zawadi moja. Hautakuwa mfanyakazi wa ndani tena. Ningependa mwanangu Khalid akuoe na uwe mkwe wangu.”

Kisha Alibaba akamgeukia Khalid.

“Yule mtu muovu ametuchezea akili zetu sote wawili mwanangu. Kwanza, aliweka alama kwenye mlango na dirisha ili aweze kurudi nyumbani hapa na kuja kuniua. Kisha akaja na kujifanya ni muuza mafuta, kumbe ndani ya mitungi yake kulikuwa na watu wenye mapanga makali! Kisha akaja kwako kwa kujifanya mfanyabishara wa vitambaa vya hariri mpaka mkawa marafiki wakubwa ilia pate nafasi ya kuwa karibu na mimi na kutimiza lengo lake. Huyu msichana wa ajabu Marjane, ameokoa maisha yetu mara zote hizo. Je utakuwa tayari kumuoa?”

Khalid akatabasamu.

“Nitamuoa Marjane, baba, kama akikubali,” Khalid alijibu. “Ni msichana mzuri, mjanja na muaminifu pia”

Kisha Khalid akamsogelea Marjane na kumshika mkono kisha akamuuliza. “Utakuwa tayari nikuoe?”

“Sawa,” Marjane alijibu.

Kisha Marjane akaangalia juu na kutabasamu kwa familia yake mpya.

Endelea sehemu ya kumi na tano ya hadithi hii…………….

 

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 123 | Added by: badshah | Rating: 0.0/0
Total comments: 1
1  
hadithii nzuri sana nimempenda sana Marjane

Name *:
Email *:
Code *: