Home » 2017 » November » 17 » Alibaba na wezi 40 Part 10
17:29
Alibaba na wezi 40 Part 10

SEHEMU YA KUMI

Kutoka sehemu ya tisa:

Baada ya mpango wa mwizi wa kwanza kufeli, ikatokea mwizi wa pili kwenda kujaribu kuitafuta nyumba ya Kassim. Kwa utaratibu uleule, mwizi wa pili alimlipa Mustafa dhahabu ili apate msaada wa kupelekwa kwenye hiyo nyumba. Sasa safari hii mwizi wa pili aliweka alama ndogo sana nyekundu ambayo si rahisi kwa mtu kuiona na kwa furaha kabisa akarudi msituni kwenda kutoa taarifa kwa kiongozi wao.

Endelea sehemu ya Kumi.

Jioni ile, Marjane alikuwa akiandaa chakula cha jioni kwa aajili ya familia ya Alibaba na wenzake nyumbani. Aliandaa nyama ya kuku, kachumbari na mchanganyiko wa mbogamboga mbalimbali, alipomaliza kuandaa mchuzi ule wa kuku na mbogamboga akaanza kuandaa upishi wa wali, alichukua sufuria na kuweka maji kiasi, kisha akaweka sufuria hiyo kwenye jiko. Baada ya hapo alienda mpaka stoo kuchukua mchele ili aweze kuchambua na kuusafisha kabla ya kuutosa kwenye maji, kwa bahati mbaya sasa, akakuta mchele hakuna.

“Itabidi tu niende kununua mchele” alijisemea moyoni. Marjane akachukua kapu lake la sokoni na kuelekea mjini sokoni.

Alipokuwa akirudi aliona alama ndogo nyekundu kwenye fremu ya dirisha, macho ya Marjane yalikuwa mazuri sana, hakuwa na matatizo ya macho hata kidogo.

“Hii alama haikuwa hapa kabla” Marjane alijisemea moyoni. “Mara ya kwanza alama nyeupe, na mara hii tena alama nyekundu!! Vizuri sana! Nitafanya kama nilivyofanya mara ya kwanza.”

Aliingia ndani na kwenda kuchukua chaki nyekundu. Kisha  akarudi nje na kuweka alama nyekundu katika kila fremu ya dirisha kwenye nyumba zote za mtaa ule.

“Hii lazima imchanganye huyu aliyeweka ile alama nyekundu pale.” Alijisemea huku akicheka. Kisha akarudi nyumbani kuendelea kuandaa chakula cha jioni, lakini hakumwambia yeyote kuhusu alama ile nyekundu.

Yule mwizi aliyeweka ile alama nyekundu alifika msituni, alipowakaribia wezi wenzake akaanza kupiga kelele za furaha, “Nimeiona! Nimeipata nyumba ambayo suti ya marehemu ilishonwa!!”

Kiongozi wao alimfurahia sana. “Umefanya kazi nzuri!” Alisema.  “Umefanya kazi muhimu sana! Sasa tunaweza kumpata aliyetuibia dhahabu zetu.”

“Nilienda mpaka kwa fundi nguo, Mustafa.” Mwizi alisema kwa kujisifu. “Alikubali kunisaidia kama ningempa dhahabu. Nikamfunga macho na kitambaa kama alivyofanya awali, na akanipeleka mpaka kwenye hiyo nyumba. Nikaweka alama ndogo sana nyekundu kwenye fremu ya dirisha ili tuweze kuipata hiyo nyumba tena.”

Wezi wakampigapiga mgongoni kama ishara ya kumpongeza huku wakishangilia. Kisha kiongozi wao akasema, “Nipeleke huko sasa hivi.”

Hivyo basi, wawili hao wakaondoka kuelekea mjini. Baada ya kufika tu mwizi mmoja akamuonesha mkuu wake nyumba ambayo kwenye dirisha kuna alama nyekundu kwenye fremu.

“Hii hapa sasa!” mwizi alimwambia mkuu wake. “hii ndiyo nyumba yenyewe! Unaona alama nyekundu kwenye fremu ya dirisha?”

Kiongozi wa wezi alienda mpaka karibu na kuiangalia alama ile.

“Ndiyo, naiona! alijibu mkuu wa wezi. “pia naona kuna alama kama hii katika fremu  ya dirisha katika nyumba ile, na ile pia! Na ile na ile! Kwanini alama hiyo ipo kila dirisha katika nyumba za mtaa huu? Nani atakuwa ameziweka hizo?”

“sijui, “ alisema mwizi yule akiwa hana furaha tena. “Mimi niliweka alama kwenye dirisha moja tu”

“wewe ni mjinga wa pili!!” alifoka mkuu wao. “haya haraka sana turudi msituni!!”

Asubuhi iliyofuata, kiongozi wao aliwaita wezi wote katika eneo lao la kukutana.

“Wawili wenu  walishindwa kuitafuta nyumba tunayoihitaji” aliwaambia. “Sasa nitakwenda na kuitafuta nyumba mimi mwenyewe. Nisubirini hapa”

Hivyo basi, kiongozi wao akaondoka kuelekea mjini mwenyewe. Akaonana na Mustafa katika kibanda chake, akampa sarafu ya dhahabu. Mustafa akamuongoza kiongozi huyo wa wezi kulekea kwenye ile nyumbaya Kassim.

Kama kawaida alivaa kitambaa kufunika macho, na kwa kutumia msaada wa harufu na sauti mbalimbali, Mustafa alifanikiwa kumfikisha kiongozi wa wale wezi mpaka kwenye ile nyumba.

“Nasikia harufu ya maua mazuri sana, natumaini hapa ndipo mahala penyewe.” Alisema Mustafa.

“Sitaweka alama yoyote ya chaki,” kiongozi yule alijisemea moyoni. “Alama za chaki zote zilizowekwa hazikuweza kufaa kabisa hapo kabla. Nitaitizama nyumba hii kwa umakini kabisa na kukariri kila kitu ili niweze kukumbuka ninachokiona.

Hivyo basi, Kiongozi yule aliangalia madirisha mazuri ya nyumba ile, pia aliangalia milango iliyopakwa rangi ya samawati na mapazia mekundu yaliyoning’inizwa kwenye madirisha. Aliangalia mimea mirefu iliyopandwa ndani ya mitungi mikubwa meupe na paka wa rangi ya machungwa mwenye macho ya njano akiwa kwenye dirisha akimtazama.

Baada ya kuangalia yote hayo, alimchukua mzee Mustafa na kumrudisha kwenye kibanda chake kisha akarudi msituni kuonana na watu wake.

“ninaifahamu nyumba ile sasa,” Alisema alipofika. “Hatuwezi kuamini alama za chaki tena, hivyo nitaamini kumbukumbu yangu. Nimeangalia kwa undani sana ile nyumba, ina madirisha mazuri sana na milango ya nje iliyopakwa rangi ya samawati, pia kuna mapazia mekundu kwenye madirisha. Nje kuna mimea mirefu iliyopandwa katika mitungi mikubwa yenye rangi nyeupe na kuna paka wa rangi ya machungwa mwenye macho ya njano anaishi humo. Itakuwa rahisi sana kuipata hiyo nyumba.”

“Sasa tunaweza kumpata mtu aliyetuibia dhahabu zetu,” kiongozi aliendelea kusema. “Na lazima tumuadhibu! Lakini kwanza, lazima tuingie ndani ya nyumba ile. Nina mpango. Tutaenda huko usiku wa leo. Njooni hapa karibu, vijana wangu, na nisikilizeni kwa makini kabisa.”

Wezi wote wakasogea karibu kusingia mpango wa kiongozi wao.

“Mtajua wenyewe mjipange vipi,” Kiongozi wao alianza kuwaambia. “Nendeni mjini na kiasi cha kutosha cha dhahabu. Jaribuni kupita kila sehemu ambayo kuna wafanyabiashara wakubwa wakubwa ambao wanatumia punda katika kazi zao. Jaribuni kuongea nao wawauzie punda, hakikisheni mnanunua punda ishirini na mniletee hapa msituni.”

Baada ya hapo wezi wakachukua kiasi cha kutosha cha dhahabu na kulekea mjini.

Endelea sehemu ya kumi na moja ya hadithi hii…………….

 

Category: Stories & Entertainment | Views: 181 | Added by: badshah | Rating: 0.0/0
Total comments: 1
1  
So interesting smile smile smile but put another story

Name *:
Email *:
Code *: